Saturday 22 August 2015

Lowassa Akwama Kuzindua Kampeni Baada ya Kukosa Uwanja wa Kutosha ‘Mafuriko’ Yake


 

Wakati mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli, akitarajiwa kuzindua kampeni zake kesho jijini Dar es Salaam, mgombea kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Edward Lowassa amekwama kuzindua kampeni zake kama ilivyotangazwa awali.

Ukawa unaoundwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), National Convention for Construction and Reform – Mageuzi (NCCR-Mageuzi), Chama cha Wananchi (CUF) na National League for Democracy (NLD) umeahirisha uzinduzi kutokana na kukosa mahali patakapotosha ‘mafuriko’ ya watu watakaohudhuria.

Lowassa alitarajiwa kufungua pazia kwa kuzindua kampeni zake kwenye Uwanja Mkuu wa Taifa jijini Dar es Salaam, lakini serikali imekataza uwanja huo kutumika kwa kampeni za vyama vya siasa.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Assah Mwambene, akiongea na waandishi wa habari Jumatano wiki hii, alisema serikali imefikia hatua hiyo kwa vile kusudio la ujenzi wa uwanja huo ni shughuli za michezo pekee na si vinginevyo.

Kampeni zinazoanza kesho pia zitahusisha wagombea urais kupitia vyama vingine vya siasa vikiwamo ambavyo wagombe wake hawapewi nafasi kubwa ya kuibua ushindani kama itakavyokuwa ama kukaribia kwa CCM na Ukawa.

Pia kuanza kwa kampeni hizi kutawahusisha wagombea ubunge na udiwani watakaoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka huu.

Afisa Habari wa Chadema iliyo mshirika katika Ukawa, Tumaini Makene, amesema kuwa, Lowassa anayewania Urais akiwa na mgombea mwenza Juma Duni Haji, ameahirisha kuzindua kampeni zake mpaka itakapotangazwa baadaye.

Alisema kuahirishwa kwa uzinduzi huo kunalengo la kutoa fursa kwa Ukawa kujiweka sawa hasa katika kupata uwanja wenye uwezo wa kuwajumuisha watu wengi na nafasi za kuegesha magari.

“Mgombea wetu hatazindua kampeni leo wala kesho, waache hao wengine waanze sisi tunajipanga kupata eneo zuri litakalotosha kwa idadi kubwa ya watu tunaowatarajia ikiwamo na maegesho ya magari,” alisema.

Makene alisema kutokana na uzeofu uliojionyesha wakati mgombea wao akitafuta wadhamini ama kutambulishwa mikoani, wanaamini kuwa mkutano wao utahudhuriwa na watu wengi, hivyo ni muhimu wakatafuta eneo kubwa la kutosha watu wengi na maegesho ya vyombo vya usafiri.

Wakati ikitarajiwa kuzindua kampeni zake kesho, CCM imeshatangaza kamati ya watu 32 kwa ajili ya kutafuta ushindi, ikiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Abdulrahaman Kinana.

Kamati hiyo ilitangazwa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, Jumanne wiki hii ambaye alimuita Kinana kama mwanaharakati wa kivita anayefahamu medani za ushindi.

Uchaguzi wa mwaka huu ambao unatarajiwa kuwa na changamoto kubwa hasa kutokana na mgombea anayeungwa mkono na Ukawa (Lowassa) akitokea CCM, kuonyesha upinzani mkubwa dhidi ya CCM alichokuwa mwanachama wake tangu mwaka 1977.

Licha ya kuwa mwanachana, Lowassa ameshika nafasi tofauti ndani ya CCM na serikalini ikiwamo Uwaziri Mkuu aliojiuzulu mwaka 2008.

Lowassa alikuwa pia katika timu ya kampeni za mwaka 2005 ambapo Rais Jakaya Kikwete aliwania nafasi hiyo kwa mara ya kwanza na kupata ushindi wa kishindo.

Hata hivyo, Julai 29, mwaka huu, Lowassa aliamua kujiunga na Chadema ikiwa ni siku chache baada ya jina lake kukatwa katika hatua za awali za kuwachuja watia nia waliotaka kuwania Urais kupitia CCM.

Jumla ya makada 42 wa CCM walijitokeza kwenye kinyang’anyiro cha kumtafuta mgombea urais ambapo 38 walirejesha fomu na Magufuli aliibuka kuwa mshindi atakayegombea Urais katika ‘kumrithi’ Rais Kikwete.

Macho na masikio ya wapiga kura wengi kuanzia kesho yataelekezwa kwenye uzinduzi wa kampeni hizo kusikia sera za vyama hivyo vikubwa vinavyoshindana kumpata Rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


from Blogger http://ift.tt/1LqybLe
via IFTTT




from WordPress http://ift.tt/1LqEn5O

No comments:

Post a Comment