Monday, 20 February 2017

MAMBO YA KUZINGATIA KABLA NA BAADA YA KUNG’OA JINO

Meno ni sehemu ya mwili ambayo hufanya kazi kubwa ikiwemo kutafuna chakula, kuongea, na kuboresha muonekano. Kwa kawaida kuna meno ya aina mbili, ya utoto ambayo huanza kuota umri wa wastani wa miezi sita, na meno ya ukubwa ambayo nayo huanza kuota wastani wa miaka sita na kuendelea. Meno hujishika kwenye mfupa maalumu ulioko kwenye taya. Meno kama sehemu nyingine ya mwili yasipotunzwa vizuri yanaweza kushambuliwa na ugonjwa wa kuoza, au ugonjwa wa fizi ambao hushambulia sehemu ambayo jino limejishika.
Kuna msemo wa Kiswahili unaosema dawa ya jino linalouma ni kungoa. Jambo hili limepelekea watu wengi wakienda hospitali wanasema nimekuja kuongoa jino. Ni vizuri kujua kuwa matibabu ya jino lenye tatizo lolote yapo, na kungoa huwa ni jambo la mwisho kabisa. Tuangalie sababu zinazoweza kupelekea daktari wa afya ya kinywa na meno ashauri jino kung’olewa.
Sababu zinazoweza kupelekea kung’oa jino/meno
• Jino lililoharibika kwa kuoza kiasi kwamba linakuwa halina nafasi ya kuliziba. Maana dawa zote zinazotumika kuziba meno, huhitaji kushikiliwa na sehemu ya jino
• Jino lililolegea kabisa (kama kutokana na ugonjwa wa fizi)
• Meno ya utoto yaliyochelewa kung’ooka na meno mengine yanataka kuota pembeni yake
• Baadhi ya watu kuwa na meno ya ziada (supernumerary teeth)
• Matibabu ya kurekebisha mpangilio wa meno wanaweza kuhitaji kung’oa baadhi ya meno ili kupata nafasi
• Watu wanaopewa tiba ya mionzi, ya kichwani na shingoni, meno yatakayopigwa na mionzi yanaweza kuhitaji kung’olewa
• Meno ya mwisho (wisdom teeth), yanapokosa nafasi ya kutosha kuota vizuri, huweza kuota vibaya hivyo kupelekea kutolewa
• Ugonjwa kwenye mfupa unaoshikilia meno kama uvimbe unaoharibu mfupa wa taya
Ni vyema kumsikiliza daktari wa kinywa na meno juu ya ushauri wa nini kifanyike. Pia unaweza kumwambia daktari nahitaji jino langu liwekewe risasi ili niweze kuendelea kulitumia. Wakati mwingine daktari anaweza kuwa anafanya kazi mahali ambapo matibabu pekee anayoweza kufanya ni kuongo’a, basi akuelekeze sehemu ambayo utaweza kupata matibabu ya kuziba meno.
Nini kinafanyika wakati wa kungo’a meno?
Kabla ya kung’oa daktari wa afya ya kinywa anaweza kushauri upige picha ya kwenye meno (kama atakuwa sehemu yenye kifaa cha eksirei ya kwenye meno), au atakuelekeza sehemu utakapoweza kupata huduma ya eksirei ya meno. Kisha daktari atakuuliza juu ya magonjwa mengine unayoweza kuwa nayo, na dawa zozote unazotumia. Hasa ukiwa na ugonjwa wa kisukari, daktari atataka kujua kama maendeleo ya ugonjwa yapoje. Kama sukari ya mwilini imepanda sana anaweza kuahirisha matibabu ya kung’oa mpaka hapo sukari itakapokuwa katika kiwango kinachotakiwa. Na tatizo la presha ya kupanda hali kadhalika.
Daktari akishajiridhisha kuwa unaweza kupatiwa matibabu ya kung’oa, basi atakuchoma sindano ya ganzi kisha kukutoa jino husika. Meno yanayotolewa kwa tahadhari kubwa ni meno yaliyoshindwa kuota vizuri (impacted teeth), na huweza kuchukua muda mrefu.
Kuna swali huwa naulizwa mara nyingi juu ya kung’oa meno ya juu na uwezekano wa kupoteza maisha au kuwa kichaa. Hakuna uhusiano wowote wa kung’oa meno ya juu ya kuwa kichaa au hata kufariki. Hiyo ni imani potofu. Baada ya kung’oa jino utapewa maelekezo ya kufuata na dawa ya maumivu. Pia daktari wako anaweza kupendekeza utumie dawa kali (antibiotic). Kwa kawaida kidonda cha jino lililong’olewa hupona haraka. Ukiona kidonda cha jino kimechukua muda mrefu zaidi ya wiki moja, rudi kwa daktari wako akaangalie tatizo ni nini, pengine kuna kipande cha jino kimebakia, au umepata tatizo baada ya kutozingatia masharti baada ya kung’oa jino.
Masharti baada ya kung’oa jino
• Ng’ata gozi iliyowekwa kwenye kidonda cha jino kwa dakika 30. Hii husaidia kuzuia damu kutoka, na kuwezesha damu kuganda. Baada ya kutoa hiyo gozi damu itaendelea kutoka kidogo kidogo hata kwa masaa kadhaa
• Usisukutue kwa maji, au dawa ya kusukutua. Hii huweza kupelekea kuondoa hiyo damu iliyoganda kwenye kidonda cha jino.
• Usile vyakula vya moto maana hii huweza kukusababishia wewe kujiunguza sehemu zilizo na ganzi, pia inaweza kusababisha damu kuanza kutoka. • Mswaki usifike kwenye kidonda cha jino siku lilipong’olewa maana inaweza kukitonesha
• Usipeleke ulimi kwenye kidonda cha jino lililong’olewa, wala kidole maana hii inaweza kupelekea kuondoa ile damu iliyoganda na hata kusababisha maambukizi kwenye kidonda cha jino.
• Pata ushauri wa daktari mara unapoona tatizo lolote baada ya kung’oa jino
Mambo ya kuzingatia kabla na baada ya kung’oa jino
• Pata kifungua kinywa kama ni asubuhi au mlo wa mchana
• Hakikisha unaeleza ukweli juu ya matatizo mengine ya kiafya kama unayo hasa ugonjwa wa presha na kisukari (kama huzingatii matumizi ya dawa ulizoandikiwa)
• Fuata maelekezo baada ya kung’oa jino. Hii itakupunguzia tatizo la kurudi hospitali ukiwa na shida iliyotokana na kungoa meno
• Rudi hospitali mara uonapo tatizo lolote limejitokeza kama damu kuendelea kutoka, kidonda cha jino kutokupona, uvimbe kuanza na kuendelea siku kadhaa baada ya kung’oa jino
• Kama wewe unavuta sigara, epuka kuvuta sigara siku ya kung’oa jino na masaa 72 baada ya kung’oa jino, hii inaongeza uwezakano wa kupata maumivu makali kutokana na kidonda cha jino kupata hali inayoitwa “dry socket”
Matatizo yasioyotarajiwa yanayoweza kutokea wakati na baada ya kuong’oa jino
• Maumivu makali kama ya jino sehemu lilipong’olewa (dry socket). Hii hutokea siku ya tatu baada ya kung’oa jino
• Kuumia kwa jino la jirani wakati kung’oa jino
• Kubaki sehemu ya jino ndani ya mfupa wake (incomplete extraction). Kwa kawaida daktari hujitahidi kuondoa sehemu yoyote ya jino inayokuwa imebakia ndani
• Kuvunjika kwa taya (hutokea mara chache sana na huwa kunakuwa na sababu)
• Kuchoka kwa misuli ya taya, hivyo kuvimba kidogo na kuuma wakati wa kufungua baada ya ganzi kuisha
• Ganzi inayochukua muda mrefu kuisha baada ya kung’oa jino. Hii huweza kutokea kama kwa bahati mbaya mshipa wa fahamu wa taya unaweza kuwa umeumizwa. Uponaji wake huchukua muda mrefu inaweza kufika miezi mitatu au zaidi. Mara chache sana ganzi hii huweza kuendelea bila kikomo.
Ukiona jambo lolote kati ya hayo hapo juu wasiliana na daktari wako wa afya ya kinywa na meno kwa ushauri zaidi.

from Blogger http://ift.tt/2l0agHV
via IFTTT




from WordPress http://ift.tt/2m0SGHJ

No comments:

Post a Comment