Thursday 20 August 2015

SOMA HII MPYA YA RAIS KIKWETE KUHUSU MAGUFULI

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Kikwete, amesema mgombea urais wa chama hicho, Dk. John Magufuli, ni chaguo la Mungu.
Akizungumza na wazee, wanawake, vijana na wanachama wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam jana, alisema jina la Dk. Magufuli lilijitokeza katika hatua zote za uteuzi ikiwamo vikao vya wazee na hata katika Mkutano Mkuu alichaguliwa na maelfu, jambo linaloonyesha anakubalika kwa wote.
Alisema Mungu ametoa hukumu yake kwa mtu wake na Watanzania ndiyo wataamua katika sanduku la kura.“Magufuli ni mgombea wa sampuli nyingine, ni mzalendo anapenda watu, nchi yake kwa dhati, asiyejikweza hana makuu, anamwamini Mungu, anatambua CCM imemfikisha alipo leo, ni kada mzoefu… sifa yake nyingine anapenda kuona matokeo ya kazi anayoifanya na aliyopewa kuifanya,” alisema.Kikwete ambaye ni Rais wa Awamu ya nne, alimwagia sifa Dk. Magufuli kuwa ni mmoja wa watumishi wa umma ambaye hakusita kutangaza Ilani ya chama chake na chama kwa ujumla, hivyo ni kada wa uhakika, mzoefu ndani ya CCM anayestahili kuunda serikali ya awamu ya tano.
“Wapo maafisa wa serikali wanaona haya kusema wanatekeleza ilani ya CCM, lakini Magufuli katika kazi zake zote alisema anatekeleza Ilani ya CCM na anatambua yupo alipo kwa sababu ya chama na siyo kwa ujanja na fedha zake kwa kuwa hana fedha,” alibainisha.
Kikwete alisema uteuzi wa Magufuli unakipa sifa chama kuwa hakinunuliki kwa kuwa hakuwahi kujivuna kwa fedha wala mali, kwani ndani ya siasa mtu anaweza kuwalipa wachache kwa tamaa na njaa zao, lakini huwezi kununua chama.
“Nawaambia watalipa wachache, lakini hawatawanunua Watanzania wataamua,” alisema na kuongeza:
“Sifa nyingine ni Mungu ametaka Magufuli awe rais, kwani aliwahi kuja Ikulu kuzungumza nami masuala ya makandarasi, nikamuuliza naona wenzako wanachukua fomu wewe huchukui?”
“Aliniuliza kwani na mimi natosha? Nilimwambia wana-CCM ndiyo wataamua kama unatosha au la,” alisema.
Alisema Dk. Magufuli ni kada aliyechukua fomu kimya kimya bila kuita waandishi wa habari.
“Alichukua fomu bila mbwembwe, alitembea kutafuta wadhamini bila wapambe na alirudisha bila mbwembwe na mgombea wa namna hiyo anakifaa chama na Watanzania,” alisema
Alisema mgombea huyo hana mbwembwe kwani alipoulizwa kama ana kikosi cha kazi, alisema anaweza kufanyakazi na yeyote na kukiachia chama kupanga timu ya ushindi ya makada 32.
Aidha, alimmimina sifa Dk. Magufuli kuwa hakubali kushindwa katika jambo lolote, mbunifu, anachukia wazembe, wababaishaji wala rushwa na kwamba atapendwa na kila Mtanzania anayechukia mambo hayo.
Kwa upande wake, Dk. Magufuli alisema anatosha pande zote, mbele, katikati, nyuma, kulia kushoto na ubavuni, na yupo tayari kupeperusha bendera ya CCM na kuongoza serikali ya awamu ya tano.
“Mwalimu alipotaka kwenda kupigana vita na Idd Amini, alianzia Dar es Salaam, marais wote waliopita walipoaanza safari ya kwenda Ikulu walianzia hapa, nimekuja kwenu wazee wa Dar es Salaam, vijana na kinamama kuomba baraka, nasaha, busara na dua zenu kabla ya kuanza safari yangu. Jumapili nitaongea mengi leo (jana) ni hayo tu,” alisema.
Alisema yuko tayari kupeperusha bendera ya CCM bila kigugumizi, kinyongo, uchovu na manunguniko hadi kuhakikisha serikali ya awamu ya tano inaingia Ikulu.
“Wana CCM tushikamane kura za maoni za urais, ubunge na udiwani zimekwisha, jukumu letu liwe kuhakikisha tunafanya kampeni uvungu kwa uvungu, kitanda kwa kitanda, chumba kwa chumba na nyumba kwa nyumba kuhakikisha CCM inaunda serikali ijayo, ni chama kikubwa kimehimili mengi na kina uwezo wa kuendelea kutawala,” alibainisha na kuongeza:
“Nawathibitishia natosha na ninatosha kweli kweli, mbele, katikati, nyuma na ubavuni, wanatosha mgombea mwenza, madiwani na wabunge.”
Shida za wana-Dar es Salaam na Watanzania nazifahamu…uzoefu wa miaka 20 serikalini unanitosha, sikuwahi kushindwa mahali.”
Mgombea Mwenza, Samia Suluhu, alisema ni mama wa watoto wanne, hivyo matatizo ya Watanzania anayajua kama mama anayeijua familia yake na kuwataka kujitokeza kwa wingi kuiunga mkono CCM.


from Blogger http://ift.tt/1Jt5I77
via IFTTT




from WordPress http://ift.tt/1LmZLJc

No comments:

Post a Comment