Baada ya Kumpa Makavu Diamond…Erick Shigongo Amgeukia Ali Kiba na Kusema Haya
Baada ya kumshauri Diamond leo nataka nimshauri Ali Kiba. Sijui kama atafurahi au atachukia, ninafanya hivi kwa kuwa sitaki waache muziki hapo baadaye huku wakiwa hawana kitu. Sitaki baadaye mtu aseme kwamba kuna watu waliwatumia, wakaingiza pesa halafu wamewakimbia.
Baada ya kusema hayo hebu niongee kilichonisukuma kuandika hiki ninachokiandika, ni ushauri, Kiba na meneja wake wanaweza kuuchukua ama kuuacha! Si lazima, kama mhamasishaji wa watu kujiondoa katika umasikini ninaona kama ninao wajibu wa kumshauri Kiba nikiwa kama kaka, anko au Mtanzania mwenzake, naamini kwa hekima walizonazo Ali Kiba na meneja wake bila shaka watapata la kuchukua, yasiyofaa wataniachia mwenyewe.
Nampenda Kiba sana tu na ninajivuna sana kuwa Mtanzania mwenzake na ningependa kuona anafanikiwa zaidi katika kazi yake. Kama siwezi kufurahi mafanikio ya Watanzania wenzangu basi hakuna haja ya mimi kuzunguka huku na kule ndani na nje ya nchi yangu kuhubiri injili ya mafanikio, watu watoke kwenye umasikini unaolitesa taifa langu.
Haikutokea tu Ali kiba akawa anapendwa vile, la hasha, ni matokeo ya vitendo fulani ambavyo amekuwa akivifanya maishani mwake mpaka Akawavuta watu kumpenda! Mambo hayo hayo akiyaacha hata followers wa Instagram wanaomfanya ajisikie anapendwa leo wataondoka!
Ali kiba, meneja wake na Watanzania wenzangu lazima mnisikilize hapa; MAFANIKIO MAISHANI HUJA NA KITU NYUMA YAKE, mara nyingi kitu hicho huwa kuwapuuza na kuwadharau waliokufikisha ulipo. Kuwatenga bila kufahamu hao ndiyo wanunuzi wa kazi zako ama wasikilizaji wa muziki wako na wakikuachia tu utatumbukia shimoni na huo ndiyo utakuwap mwisho wako.
No comments:
Post a Comment