Tuesday 13 October 2015

Mkutano wa Tume na Viongozi wa Vyama vya Siasa katika Ukumbi wa New Africa Hotel.


  HOTUBA YA UFUNGUZI YA MWENYEKITI WA TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI KATIKA MKUTANO WA TUME NA VIONGOZI  WA VYAMA VYA SIASA KATIKA UKUMBI WA NEW AFRICA HOTEL TAREHE 12/10/2015.
Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Mheshimiwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa Ya Uchaguzi,
Waheshimiwa Makamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi,
Mkurugenzi wa Uchaguzi,
Inspekta Jenerali wa Polisi,
Msajili wa Vyama vya Siasa,
Viongozi wa Serikali,
Watendaji wa Mradi wa Uimarishaji wa Demokrasia (DEP),
Watendaji wa Tume,
Waandishi wa Habari,
Mabibi na Mabwana.
Kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, napenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisheni wote katika Mkutano huu wa kujadiliana na kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali  ya  Uchaguzi pia  kupeana taarifa kuhusu maandalizi ya Uchaguzi Mkuu utakaofanyika tarehe 25 Oktoba 2015.
Pamoja na kwamba mna majukumu mengi na ya muhimu mmetambua umuhimu wa mkutano wetu na mmekuja kuhudhuria mkutano huu kama ilivyotarajiwa. Tume imefarijika  sana kukutana nanyi siku ya leo na tunawashukuru kwa moyo mliyoonyesha katika mchakato huu wa maandalizi ya Uchaguzi na wa kututhamini na kuja kuhudhuria Mkutano wetu.
Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Pamoja na changamoto mbalimbali mnazokabiliana nazo  katika kutekeleza majukumu yenu kisiasa  ni ukweli ulio dhahiri, kuwa Viongozi wa Vyama vya Siasa ni Wadau  muhimu wa  Uchaguzi ambapo  mkishirikiana kutekeleza majukumu yenu kwa ufasaha mtaleta mafanikio katika uendeshaji wa Uchaguzi.
Viongozi wa Vyama vya Siasa,
Vyama vya Siasa vina nafasi kubwa katika kuelimisha na kuhamasisha jamii, Tume inaamini kwamba ili Mpiga Kura aweze kufanya maamuzi sahihi ni muhimu kwake kupate Elimu sahihi. hivyo basi, Tume inatarajia kuona mkitumia majukwaa yenu vyema katika kuhamasishaji na kuelimishaji si tu wanachama wenu bali jamii nzima ya watanzania
Viongozi wa Vyama Vya Siasa
Kuelekea Uchaguzi Mkuu, Tume imeaandaa vituo vya kupigia kura 64,736, ambapo, Tanzania Bara ni Vituo 63, 156 na Zanzibar ni Vituo 1,580. Kila kituo kitakuwa na uwezo wa kuhudumia  Wapiga Kura  450 na wasiozidi 500. Hata hivyo Kituo kinapokuwa na  wapiga Kura zaidi ya 500 kinabidi kigawanywe ili viwe viwili yaani Kituo “A” na Kituo “B” na namba ya Wapiga Kura itakuwa nusu kwa nusu.  Wapiga Kura wanashauriwa kwenda katika vituo walivyojiandikishia kupiga kura siku nane (8)  kabla ya siku ya kupiga kura ili kuweza kujua Vituo vyao halisi vya kupigia kura.  Sambamba na hilo wananchi wataweza kupata taarifa zao zilizoko kwenye kanzidata (Database) kwa kutumia simu zao za kiganjani kupitia ujumbe mfupi wa maneno ‘sms’ bila wao kulazimika kufika vituoni, namba hiyo ni *152*00# na kufuata maelekezo. Au kupitia Tovuti ya Tume ambayo ni (www.nec.go.tz)

Viongozi wa Vyama Vya Siasa,
Tume imekuwa ikifuatilia kampeni za Vyama vyenu vya Siasa, hata hivyo Tume inasikitika kuona kuwa baadhi ya Vyama vya Siasa vimekuwa vikitumia majukwaa yao vibaya. Tume kwa namna ya pekee inawaomba katika kipindi hiki kifupi kilichobaki kutumia nafasi zenu majukwaani kuelezea sera za Vyama Vyenu ili kuweza kuwasaidia wananchi kufanya maamuzi sahihi baada ya kuwa na taarifa sahihi.
Viongozi wa Vyama Vya Siasa,
Tume imekuwa ikisikia katika vyombo vya Habari malalamiko mengi kuhusu uvunjifu wa maadili ya Uchaguzi katika kipindi hiki cha kampeni, naomba nitumie nafasi hii kuwaasa viongozi wa vyama vya siasa kupeleka malalamiko yenu  katika kamati za maadili na si kukimbilia katika Vyombo vya Habari kama ambavyo baadhi ya Vyama vya Siasa na Wagombea mmekuwa mkifanya.
Viongozi wa Vyama Vya Siasa
Tume inawaomba kuepuka kutoa taarifa na shutuma sisizo sahihi kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi badala yake mjikite katika kufikisha taarifa zilizo sahihi na zilizokusudiwa kwa Wafuasi wenu na wananchi wote kwa jumla, na pia kuwahamasisha wananchi kujitokeza kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba 2015.
Viongozi wa Vyama Vya Siasa,
Tume imejipanga kuhakikisha kila Mpiga kura  mwenye sifa za Kupiga Kura anapiga Kura yake pasipo kubughudhiwa. Ili kuhakikisha jambo hili linafanyika kwa ufanisi, Tume imetoa maelekezo kwa Makarani waongozaji vituoni kutoa upendeleo kwa watu wanaoishi na Ulemavu ili kuwasaidia waweze kupiga kura. Kwa wale wasioona Tume imeandaa kifaa maalumu cha nukta nundu ‘Tactile Ballot Folder’ ambayo itawasaidia katika upigaji kura kwa urahisi.
Viongozi wa Vyama Vya Siasa
Baadhi ya wagombea wamekuwa wakiwashawawishi Wapiga Kura wao kutoondoka katika Vituo vya Kupigia Kura baada ya kumaliza zoezi la Upigaji Kura, naomba nichukue nafasi hii kuwakumbusha kifungu cha 104 (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kinasema nanukuu
Hakuna mtu atakayefanya Mkutano siku ya kupiga kura katika au ndani ya jengo lolote ambamo upigaji kura katika Uchaguzi unaendelea, au mahali popote ndani ya eneo la mita 200 ya jengo hilo, kuvaa au kuonyesha kadi ya picha yoyote, upendeleo au nembo nyingine inayoonyesha kuunga mkono mgombea Fulani katika Uchaguzi.“  mwisho wa kunukuu.
Aidha, kifungu cha 103 (1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292 kinasema, nanukuu:
“Hakuna mtu atakayeruhusiwa, katika jengo lolote ambalo upigaji kura katika Uchaguzi unaendelea, au njia yoyote inayotumiwa na umma ndani ya umbali wa mita tatu ya mlango wowote wa kuingilia katika jengo atavaa au kuonyesha au kuonyesha kadi, upendeo au nembo yoyote inayoashiria kumuunga mkono mgombea Fulani katika Uchaguzi” mwisho wa kunukuu.
Kifungu cha 5 cha Sheria ya Adhabu, Sura Na. 16 kinaeleza maana ya njia ya Umma. Nanukuu:
“Public way includes any highway, market place, square, street, bridge or other way which is lawfully used by the public”  Mwisho wa kunukuu.
Vifungu vya Sheria zote kwa pamoja havisemi wala kutoa fursa au nafasi kwa wananchi kukusanyika, zinapiga marufuku na kukataza uvaaji wa sare, au nembo au alama za Vyama vya Siasa siku ya kupiga kura kwa umbali kati ya mita 200 na 300.
Hivyo basi ieleweke kwamba umbali huo wa mita 200 mpaka 300 sio umbali unaowaruhusu watu kukusanyika kwa kisingizio cha kulinda kura.
Hivyo niwaase Wanasiasa kuzingatia Sheria na taratibu za uendeshaji wa Uchaguzi,  kuepuka lugha zozote za uchochezi zinazoweza kuleta uvunjifu wa amani na kuhatarisha maisha ya Watanzania.  Aidha uzoefu unaonyesha kwamba, katika Kampeni zinazoendelea, pale ambapo wafuasi wa Vyama tofauti wanapokutana uwezekano wa kutokea vurugu ni mkubwa na sehemu nyingine vurugu zimetokea na kusababisha maafa, majeruhi na uharibifu wa mali.
Hivyo, endapo kila chama kitaamua kuwaelekeza wafuasi wake kubaki kwenye Vituo vya Kupigia Kura uwezekano wa kutokea vurugu ambazo zinaweza kupelekea kuwatisha, kuwabughudhi, kuwatia hofu na kuwasumbua Wapiga Kura ni mkubwa hivyo kuhujumu zoezi la Upigaji Kura,
Zaidi ya hayo, maelekezo yaliyotolewa chini ya kifungu cha 126 na kifungu cha 63(2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 63(2) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura 292 na kifungu2.1 cha Maadili ya Uchaguzi ya mwaka 2015 yanasistiza kwamba kiongozi yeyote wa Chama cha Siasa anapaswa kuheshimu na kufuata maagizo yote ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Viongozi wa Vyama Vya Siasa
Kwa kumalizia ninapenda tena kuwashukuru wote kwa kuhudhuria Mkutano huu na Tume inaahidi kuyachukua mawazo yenu na kuyafanyia kazi yale yaliyomo ndani ya uwezo wetu ili kuweza kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa mwaka  2015 kwa amani na utulivu.
Baada ya kusema hayo kwa niaba ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, natamka kuwa Mkutano huu umefunguliwa rasmi.
Asanteni sana kwa kunisikiliza.

HAKIKI KADI YA MPIGA KURA
http://ift.tt/1LrMRIHvote 
SMS
+255(0)772 55 55 53
LISTEN LIVE
http://ift.tt/1jVc3owFocusRadioTz
Tume ya Taifa Ya Uchaguzi Tanzania
YOUTUBE / TV
http://bitly.com/1Leujup
VIPINDI VYA REDIO
http://bitly.com/1Clt0r8 

FACEBOOK
http://bitly.com/1zIiIkq 

TWITTER
http://bit.ly/1678Vq2

 Mkurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Tanzania akizungumza na Viongozi wa Vyama vya Siasa Tanzania katika ukumbi wa Hoteli ya New Afrika Hoteli Jijini Dar es Salaam.wakati mkurugenzi wa Tume ya Uchgaguzi Tanzania akitowa Taarifa ya Tume kwa Viongozi hao. 
Viongozi wa Vyama vya Siasa Tanzania wakifuatilia mkutano wa Tume ya Uchaguzi Tanzania wakati Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Lubuva akihuitubia na kutoa taarifa kwa Viongozi wa Siasa katika ukumbi wa hoteli ya New Afrika Dar es Salaam.
Viongozi wa Vyama vya Siasa Tanzania wakifuatilia mkutano wa Tume ya Uchaguzi Tanzania wakati Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Jaji Lubuva akihuitubia na kutoa taarifa kwa Viongozi wa Siasa katika ukumbi wa hoteli ya New Afrika Dar es Salaam. 

from Blogger http://ift.tt/1WYRIox
via IFTTT




from WordPress http://ift.tt/1LiadwQ

No comments:

Post a Comment