Monday 19 January 2015

Wabia wa Maendeleo watia sahini kuisaidia SAGCOT


Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Bibi Sophia Kaduma akitia sahini utekelezaji wa pamoja kati ya Serikali ya Tanzania na Wabia wa Maendeleo ili kusukuma kwa pamoja malengo ya SAGCOT, kushoto kwake ni Bibi, Hanne- Marie Kaarstad, Msimamizi Mkuu wa maendeleo kutoka Ubalozi wa Norway na anayefuatia ni Bwana Eric Beaume, kutoka Idara ya Mahusiano ya Jumuia ya Ulaya.
Wabia wa Maendeleo wakiongozwa na Bwana Philippe Dongier, Mkurugenzi Mkazi wa Bank ya Dunia nchini, leo wametia sahini ya makubaliano ya kuisaidia SAGCOT, makubaliano hayo ni utekelezaji wa ahadi za wabia hao ili kufanikisha utekelezaji wa majukumu ya Mpango huo.
SAGCOT ni kifupi cha maneno, chenye maana ya Southern Agricultural Growth Corridor Growth of Tanzania tafsiri yake ni Mpango wa Kuboresha Kilimo Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini ilianzishwa miaka mitatu iliyopita leo lake kubwa na kusaidi uwekezaji mkubwa na mdogo katika kilimo kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Awali katika hotuba yake ya ufunguzi wa tukio hilo, Katibu Mkuu, Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika, Bibi Sophia Kaduma alisema kutiliana sahini ni mwanzo mzuri, kwani Serikali kwa kushirikia na sekta binafsi, maendeleo katika sekta ya kilimo yatafikiwa kwa haraka.
Bibi Kaduma alisema, lengo la Serikali ni kupunguza umaskini, kuboresha maisha ya watu vijijini na mijini na kuongeza kuwa kiasi cha dola bilioni 2.1 za Marekani ambazo zitawekezwa kupitia Mpango huo zitachangia katika ukuaji wa uchumi kupitia kilimo.
Naye Bwana Vel Gnanendran, Mwakilishi wa Mkazi wa DFID alisema huu ni mwanzo mzuri na tukio la kutiliana sahini ni mwanzo mzuri na kwamba wabia wa maendeleo wapo mstali wa mbele kuhakikisha, malengo ya SAGCOT yanafikiwa ikiwa ni pamoja na kuboresha utendaji kazi wa Mpango huo.
Bwana Geoffrey Kirenga, ambaye ndiye Mtendaji Mkuu wa SAGCOT alisema, Mpango huo unatekelezwa kwa pamoja kati Serikali kwa kushirikiana na wabia wa maendeleo na kuishukuru Serikali kwa kuja na mtazamo mpya wa kuishirikisha Sekta binafsi katika kukuza na kuendeleza uchumi wa Taifa.
Bwana Kirenga aliongeza kuwa, sasa ni wakati wa kila Mtanzania kubadili fikra kwa kuwa, maendeleo yanaletwa kwa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi, na kushauri Watanzania kuacha fikra za kusubiri kusaidiwa.
Bwana Kirenga alisema mpaka sasa, wabia wa maendeleo wametoa ahadi ya kiasi cha Dola za Kimarekani, bilioni 1 ambazo zitatolewa punde ili kuanza utekelezaji katika eneo la usimamizi na uratibu wa shughuli za SAGCOT.


WAZIRI AFANYA ZIARA MKOANI MBEYA
Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika amefanya ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mbeya kukagua shughuli mbalimbali za kilimo mkoani humo, akiwa wilayani mbarali waziri aliwataka watendaji wa Halmashauri kushiriki kikamilifu katika utekelezaji wa mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN).Vilevile ameagiza kuundwa kwa timu ya wataalamu kuchunguza sababu za kubomoka bwawa la lwanyo lilopo katika kata ya Igurusi wilayani mbalali.
Akiwa wilayaniMomba aliwataka wanakijiji wa kijiji cha Ukwile kata ya Isandula kutumia fulsa ya mipaka ya nchi za jirani kama Malawi na Zambia katika kupata masoko ya mazao yao pia Halmashauli na sekta binafsi kutatua changamoto za fedha zinazowakabili.
Waziri akiwa wilayani Mbozi alikagua maendeleo ya ununuzi wa mahindi unaofanywa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Wilayani humo.

Zambi : Wahujumu wa Ushirika Kukiona

Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mheshimiwa Godfrey Zambi akipata maelezo toka kwa viongozi wa wilaya ya Mvomero
Naibu Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika Mheshimiwa Godfrey Zambi amesema serikali itachukua hatua kali kwa watu wote watakaohusika na kuhujumu vyama vya ushirika hapa nchini.
Mheshimiwa Zambi aliyasema hayo wakati akitoa salamu zake katika ziara ya Waziri wa Kilimo Chakula na Ushrika Mheshimiwa Eng. Christopher Chiza mkoani Morogoro.
“ Viongozi wa vyama vya ushirika ndio tatizo Kubra katika ustawi wa ushirika hapa nchini kwani wamekuwa chanzo cha kuhujumu ushirika” aliongeza Mhe. Zambi.
Wamekuwa wakitumia nafasi zao za uongozi kwa kujipendelea katika utoaji wa mikopo,  alisisitiza Mheshimiwa Zambi katika hotuba yake.
“ Tumetunga sheria namba 6 ya Ushirika ya mwaka 2013 itakayowabana viongozi hawa wa ushirika wanaokwenda kinyume na uendeshaji wa ushirika” alifahamisha Mheshimiwa Zambi.
Sheria hii ni kali sana na itawabana kikamilifu wanaohujumu ushirika  na hivyo kurudisha nyuma nia ya wananchi kuwa na maisha bora, aliongeza.
Alisema  tatizo lingine linalokwamisha na kuathiri ushirika ni utitiri wa vyama vya ushirika katika sehemu moja.
Kuna vyama vya ushirika ambavyo havifanyi kazi iapasavyo katika kuendeleza ushirika wetu bali vinakuwepo kwa jina tu.
“ Kuna umuhimu  kuwa na vyama vichache vyenye ufanisi kuliko ilivyo sasa ambapo kuna mlundikano vyama usio na tija kwa wanaushirika” alifahamisha Mhemiwa Zambi.
KILIMO CHA UMWAGILIAJI KUCHANGIA ASILIMIA 25 YA CHAKULA

Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, Mheshimiwa Eng.  Christopher Kajoro Chiza (Mb) ameeleza  kuwa, kilimo cha umwagiliaji  kina nafasi ya kuchangia asilimia 25 ya chakula  kinachozalishwa nchini.  Aliyalisema hayo wakati  alipotembelea mradi wa umwagiliaji wa Nkoanrua katika Halmashauri ya  Wilaya ya  Meru.
Azma hiyo inaweza kufikiwa kwa  kuongeza eneo,   pamoja na kuongeza tija katika maeneo yaliyopo. Hatua za kuchukua ni pamoja na kubadili kilimo cha kujikimu kuwa cha kibiashara.
Alisisitiza kuwa hatua hiyo itafikiwa endapo wakulima watabadilika na  kulima kilimo cha kisasa badala ya  kilimo cha mazoea.
Hatua nyingine ni kukarabati na kuisafisha mifereji  ya umwagiliaji iliyopo kwa lengo la kupunguza upotevu wa maji ili kuleta ufanisi katika matumizi ya maji.  Vile vile aliwahimiza wakulima kuzalisha mara mbili katika msimu, aliongeza Mheshimiwa Chiza.
Aidha, alihimiza umuhimu wa kulinda vyanzo vya maji na kuwa na Kamati ya watumia maji ili kuboresha huduma za umwagiliaji.
Hatua hizo zitawezesha kufikiwa kwa malengo ya Matokeo Makubwa Sasa (BRN) ambapo ifikapo  mwaka 2015 kuwe  na ongezeko la mavuno  kwa  zao la mahindi la tani 100,000, mchele tani 290,000 na Sukari tani 150,000.

WIZARA YAENDESHA MAFUNZO

Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika imeendesha  mafunzo ya usimamizi na uhifadhi wa zao la mpunga baada ya mavuno,  yaliyofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Edema katika Manispaa Morogoro kuanzia tarehe 20 – 31 Januari, 2014.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idara ya Zana  Eng. Mark Lyimo, Mafunzo hayo yaliwwahusisha Maafisa Zana na Ugani wapatao 14 na wakulima 84 kutoka skimu 14 za umwagiliaji wa Halmashauri za Mikoa ya Mbeya, Morogoro, Tanga, Arusha, Iringa, Kilimanjaro Manyara na Ruvuma.
Pia katika mafunzo haya taasisi binafsi ya RUDI ilishiriki ikiwa ni katika harakati za  kushirikisha  sekta binafsi katika kuboresha kiilimo hapa nchini.
Baadhi ya mada zilizowasilishwa katika mafunzo haya ni pamoja na  uzalishaji kitaalam,  usindikaji wa zao la mpunga na kanuni zake, Uhifadhi bora wa zao la mpunga, ufungashaji na kupiga chapa bidhaa za mpunga katika kulenga soko, alifafanua Eng. Lyimo.
“Lengo kubwa la mafunzo haya ni kutoa elimu kwa maafisa zana na wakulima kwenye skimu za umwagiliaji ili waweze kutumia teknolojia za kisasa katika kuzalisha, kuvuna na kuhifadhi katika kuongeza thamani kwa lengo la  kuboresha na kuongeza tija kwa mkulima mdogo katika maeneo ya umwagiliaji hapa nchini” aliongeza Eng. Lyimo.
Mada  nyingine ni kanuni bora za uzalishaji wa zao la mpunga, usindikaji,  matumizi sahihi ya mashine  bora katika kilimo cha mpunga zitakazotolewa na Serikali katika skimu 14 chini ya Mradi wa Sera na Maendeleo ya Rasilimali Watu (PHRD), alifafanua Eng.  Lyimo.
Mafunzo haya ni sehemu ya utakelezaji wa mpango wa  Serikali wa Matokeo Makubwa  Sasa (BRN) kwa Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika ambapo zao la mpunga  ni mojawapo linalopewa kipaumbele katika kuongeza uzalishaji na tija.

Taasisi za Wizara ya Kilimo zatakiwa Kupunguza na Utegemezi
Wakuu wa Taasisi za Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika walipokutana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bibi Sophia Kaduma hivi karibuni katika ukumbi wa Kilimo I
Taasisi zilizopo chini ya Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika zimetakiwa kuwa na mikakati ambayo itaziwezesha kujitegemea katika  shughuli zao  ili kupunguza utegemezi katika mfuko wa serikali.
Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu wizara ya kilimo chakula na ushirika Bibi Sophia Kaduma katika Kikao  kilichojumuisha Wakuu wa taasisi hizo  kilichofanyika katika ukumbi wa Kilimo I hivi karibuni
Akiwasilisha taarifa yake Bibi Sophia amezitaka kila Taasisi kuainisha vyanzo vyake vya mapato   nje ya ruzuku  ya serikali  ikiwemo michango ya wadau . ‘kila Taasisi kwa namna moja au nyingine inakusanya mapato yake, “nataka kila mkuu wa Taasisi aainishe  vyanzo vyake vya fedha anavyotegema kukusanya katika mwaka 2014/15” alisema Bibi Kaduma.
Aidha katika kikao hicho wakuu wa taasisi walipata fursa ya kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kuendesha taasisi hizo pamoja na ubunifu wa kujipatia fedha kutokana na rasilimali zake.
Pamoja na hayo Katibu Mkuu alisisitiza kuwa vikao vya namna hiyo vitakuwa vinafanyika angalau kila robo mwaka ili kuongeza ufanisi katika kusimamia taasisi hizo.

WAZIRI WA KILIMO CHAKULA NA USHIRIKA AMESEMA HAPENDI KUONA TASNIA YA SUKARI IKIKOSA MWELEKEO
"Mhe. Eng. Christopher Kajoro Chiza Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika akitoa hotuba kwa Wadau wa Sukari katika Mkutano uliofanyika Mjini Morogoro Mwanzoni mwa Januari 2014.

Mhe. Eng. Christopher Kajoro Chiza (Mb) Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika ameonya kuwa kuwa Serikali haitapenda kuona Tasinia ya Sukari ikikosa mweleleo kutokana na matakwa ya kundi fulani. Alisisitiza kuwa, Tasnia ya sukari ni moja ya tasnia kubwa nchini ikijumuisha wadau muhimu wakiwamo walaji, wakulima, wafanyabiashara na wazalishaji. Kila mdau katika jumuisho hili ana maslahi ambayo kwa namna moja au nyingine yanaweza kukinzana na ya mdau mwenzake. Mkulima angependa kuona anauza miwa yake kwa bei ya juu, hali kadhalika mzalishaji kuuza sukari anayozalisha kwa bei yenye faida ya kutosha. Aidha mfanyabiashara angependa kupata faida maradufu na panapokuwa na mwanya kuingiza sukari kutoka nje kwa njia sizizo halali. Lakini kwa upande mwingine mlaji naye angependa kununua sukari kwa bei nafuu.
Serikali haipo tayari kuona tasnia kubwa na muhimu kama hii ya sukari ikipoteza mwelekeo, aidha ingependa kuwepo kwa mazingira mazuri (win - win situation) kwa kila mdau. Kwa maana hiyo nimeona ni jambo jema na muhimu sana kuwakutanisha ninyi wadau ili tuweze kujadili kwa pamoja changamoto zilizopo mbele yetu juu ya sekta hii. Ni matarajio yangu kwamba, mkutano huu utaweka misingi ya kufikia utatuzi wa chamngamoto hizi kwa manufaa ya pande zote
Mhe. Waziri ameyasema hayo katika mkutano wa Wadau wa Sukari uliofanyika Mjini Morogoro mwanzoni wa mwezi Januari
Akitoa picha halisi ya uzalishaji na mahitaji ya sukari hapa nchini Waziri Chiza alisema kuwa, Wakati viwanda vyetu vinabinafsishwa vilikuwa vinazalisha wastani wa tani 120,000 kwa mwaka. Sasa uzalishaji umefikia wastani wa tani 300,000 kwa mwaka.
Aidha uzalishaji wa miwa (siyo sukari) katika mashamba ya wakulima wadogo nao umeongezeka kwa asilimia 61 (hii ni kutoka wastani wa uzalishaji wa tani 439,122 hadi tani 705,176 kwa mwaka). Uzalishaji katika mashamba ya wenye viwanda umeongezeka kutoka wastani wa tani 1,083,738 na kufikia tani 2,229,274 kwa mwaka (ongezeko la asilimia 105).
Pamoja na mafanikio haya bado tasnia ya sukari imegubikwa na changamoto mbali mbali kubwa zaidi ikiwa uzalishaji usiokidhi mahitaji. Mahitaji yetu ni wastani wa tani 590,000 za sukari kwa matumizi ya kawaida na ya viwandani. Viwanda vya sukari nchini huzalisha takribani asilimia sabini tano (75%) ya mahitaji ya sukari ya matumizi ya kawaida. Wastani wa tani 290,000 ni nakisi inayojazwa na uagizaji sukari kutoka nje. Nakisi hii inajumuisha sukari ya matumizi ya kawaida (gap sugar) ya wastani wa tani 120,000 na sukari ya matumizi ya viwandani ya wastani wa tani 170,000 kwa mwaka. Kiasi chote cha sukari ya matumizi ya viwandani kinaingizwa nchini kutoka nje. Aidha uagizaji wa sukari ya matumizi ya kawaida unategemea hali halisi ya soko kwa kipindi husika na kwa hiyo uagizaji halisi unaweza kuwa juu au chini ya nakisi hiyo. Hata hivyo, Kamati ya Ufundi ya Ushauri ya Uagizaji Sukari iliyokutana tarehe 24/12/2013 kujadili hali ya sukari nchini imependekeza kuwa mwaka huu 2013/2014 kusiwe na uagizaji wa sukari kwa sababu kiasi tha tani 257,000 kitapatikana kwa matumizi ya kawaida kuanzia sasa hadi mwishoni mwa 2013/2014.
ZIARA YA WAZIRI MTWARA

Mhe. Eng. Christopher K. Chiza (MB) Waziri wa Kilimo Chakula na ushirika akikagua ujenzi wa ghala la TANECU (Tandahimba Newala Cooperative Union) Ghala hilo litakuwa na uweza wa kuhifadhi tani 10,000 za korosho na linajengwa Tandahimba . Ghala hilo ni maandalizi ya ujenzi wa kiwanda cha kubangulia korosho kitakachojengwa na TANECU.

Mhe. Eng. Christopher K. Chiza (MB) Waziri wa Kilimo Chakula na Ushirika, akipata maelezo ya zana inayotumika kuandaa mashamba ya mpungaa katika kijiji cha Mahuninga wilaya ya mtwara. Mashamba hayo yenye ukubwa wa ekari 1,000 yanalimwa na mwekezaji mzalendo Bw. Hamis Ismail Msigwa ambaye anashirikiana na vijiji vya Mahuninga na kitunguli.

Mhe. Eng Christopher K. Chiza (MB) akikagua shamba linaloandaliwa kwa ajili ya kilimo cha mpunga katika kijiji cha Mahuninga katka Wilaya ya Mtwara. Mashamba hayo yanamilikiwa na mwekezaji mzalendo Hamis Ismail Msigwa

No comments:

Post a Comment