Wednesday, 12 April 2017

HUKU Wananchi Wakilalamikia Uchumi…Ripoti Benki ya Dunia Yaipaisha Tanzania

RIPOTI ya tisa ya Hali ya Uchumi wa Tanzania ya Benki ya Dunia imeitaja Tanzania kuwa ni nchi inayoendelea kufanya vizuri katika ukuaji wake wa uchumi, ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Tanzania ni nchi ya kwanza ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya vizuri kiuchumi huku katika ukanda wa nchi za Jangwa la Sahara ni miongoni mwa nchi tatu zikiwemo Rwanda na Ethiopia zinazofanya vizuri kiuchumi.
Hayo yalibainishwa na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Somalia, Burundi na Malawi, Bella Bird jijini Dar es Salaam jana wakati ripoti hiyo ilipowasilishwa mbele ya wadau mbalimbali wa uchumi nchini.
Alisema pamoja na kwamba katika kipindi cha mwaka jana nchi nyingi za Afrika, zikiwemo za kusini mwa Jangwa la Sahara zilikabiliwa na kushuka kwa kasi kwa uchumi kunakokadiriwa kuwa ni kwa asilimia 1.5, Tanzania imeendelea kuonesha ustahimilivu wa kiuchumi katika kipindi chote hicho.
“Viwango vya ukuaji wa uchumi Tanzania vinaendelea kuzipiku nchi za jirani za Afrika Mashariki. Ustahimilivu huu unatokana na sifa kadhaa za uchumi wa Tanzania,” alifafanua.
Alisema kwa mujibu wa ripoti hiyo inaonesha uchumi wa Tanzania kuanzia mwaka 2011 ulikuwa kwa asilimia 7.9, mwaka 2012 asilimia tano, 2013 asilimia saba, 2014 asilimia 6.7, 2015 asilimia 6.7 na mwaka jana asilimia saba.
Aidha ripoti hiyo kwa upande wa Kenya ilionesha mwaka 2011 uchumi wake ulikua kwa asilimia sita, 2012 asilimia 4.7, 2013 asilimia 5.5, 2014 asilimia 5.2, 2015 asilimia 6.8 na mwaka jana asilimia 6.8 wakati Uganda mwaka 2011 ulikuwa kwa asilimia 6.8, 2012 asilimia 3.9, 2013 asilimia nne, 2014 asilimia 5.2, 2015 asilimia 6.5 na mwaka jana asilimia 4.9.
Alisema Tanzania ina vyanzo anuai vya ukuaji ambapo takribani robo ya pato lake ghafi la taifa linatokana na kilimo na nusu nyingine inatokana na sekta tano ambazo ni biashara ya jumla na rejareja, ujenzi, uzalishaji, viwanda, uchukuzi na utawala wa umma.
“Hali ya uchumi wa Tanzania iko imara lakini hakuna nafasi ya kubweteka kwani imedhamiria kuendeleza viwango vya sasa vya ukuaji vya takribani asilimia saba na kufikia asilimia 10 kama ilivyo lengo la serikali ifikapo mwaka 2020/21 katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea kwenye uchumi wa viwanda,” alisema.
Alisema nchi hiyo imefanya vizuri kwa kuendelea kuwa na sera makini za uchumi mkuu ambapo mwaka jana shilingi ya Tanzania ilikuwa imara kutokana na kuwepo kwa akiba ya kutosha huku mfumuko wa bei ukibaki katika kiwango cha chini ya wastani ambacho ni asilimia 5.5 ikilinganishwa na mwaka 2015.
Bird alisema kwa upande wa fedha, serikali ya Tanzania inastahili pongezi kwa kuongeza makusanyo ya mapato ya ndani hadi kufikia asilimia 14.5 ya pato ghafi la taifa kupitia jitihada za kupunguza misamaha ya kodi na kudhibiti rushwa.
“Kwa kweli uongozi wa Tanzania unahitaji pongezi kwa hili, lakini changamoto zimeonekana katika kugharamia bajeti ya maendeleo na mzigo wa madeni umeshughulikiwa kwa sehemu ndogo, hali iliyoleta athari kwa wawekezaji kukosa imani lakini pia sekta binafsi kutoshirikishwa vyema,” alifafanua.
Hata hivyo, alitaja sekta ambazo ikilinganishwa na mwaka 2015, mwaka jana na mwaka huu zinaendelea kukua nchini humo kuwa ni sekta ya ujenzi kwa asilimia 18, madini na uchimbaji mawe asilimia 16.5, usafirishaji na uhifadhi asilimia 17, habari na mawasiliano asilimia 14 na fedha na bima asilimia 12.
Alitaja sababu zingine za nchi hiyo kufanya vizuri kiuchumi kuwa ni tangu Rais John Magufuli aingie madarakani mwaka 2015, aliingia na sera kali iliyolenga kuimarisha utawala wa umma, kudhibiti rushwa na kuimarisha usimamizi wa kodi hali iliyosaidia kuiongezea mapato ya ndani nchi hiyo.
Alipongeza juu ya hatua iliyofikiwa ya kuhakikisha huduma ya upatikanaji wa fedha kwa wote inafikiwa ambapo kwa sasa kutokana na matumizi ya huduma za kibenki kwa njia ya simu zimewezesha idadi kubwa ya watanzania kufikiwa na huduma ya fedha tofauti na miaka ya nyuma.
Alisema mwaka 2006 kulikuwa na asilimia 11 tu ya watu wazima wanaotumia simu za mkononi lakini tangu kuanza kutumika kwa huduma za kibenki kwa njia ya simu mwaka 2008 kwa sasa jumla ya asilimia 62 ya watanzania wana akaunti za benki kupitia kampuni za simu kwa kushirikiana na taasisi za fedha.
Aidha, alisema uchumi huo umeendelea kuimarika ingawa kumekuwepo kwa changamoto za kudhibiti matumizi ya fedha ambayo kwa namna moja yamekuwa yakiikandamiza sekta binafsi inayotegemea zaidi serikali kama mteja wake mkuu.
Alitaja mafanikio na maeneo ambayo matumizi ya fedha yamebanwa kuwa ni pamoja na uamuzi wa Dk Magufuli kuzuia matumizi yasiyo ya lazima ikiwemo safari za nje ya nchi, kupunguza malipo yasio ya lazima ya posho, kufichua watumishi hewa kwenye sekta ya umma ambao takribani 15,000 walibainika na kupiga marufuku mikutano kufanyikia kwenye mahoteli.
Alitaja changamoto nyingine zinazoikabili sekta ya uchumi kuwa ni kuendelea kuwepo kwa tatizo la ajira ambapo kwa sasa inakadiriwa kuwepo kwa vijana 800,000 wanaoingia kwenye soko la ajira kila siku.

from Blogger http://ift.tt/2o4dyuk
via IFTTT




from WordPress http://ift.tt/2oy6yKm

No comments:

Post a Comment