Jana mjadala mzito umeibuka kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari baada ya Rais Dkt Magufuli kufuta kauli ya Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt Harrison Mwakyembe iliyokuwa ikitaka wananchi wote kuwa na vyeti vya kuzaliwa kabla ya kufunga ndoa.
Waziri Mwakyembe akitoa tamko hilo alisema kuwa, hakuna ndoa yeoyote itakayofungwa iwe ya kimila, kiserikali au kidini ambayo wahusika wake watakuwa hawana vyeti vya kuzaliwa.
Akieleza dhumuni la uamuzi huo, Waziri Mwakyembe alisema serikali imeamua kufanya hivyo ili kupata takwimu sahihi za wananchi wake zitakazosaidia kupanga mipango ya kimaendeleo sanjari na kuzuia wageni kuingia kinyemela nchini.
Jana asubuhi kabla ya kuaza safari ya kurejea Dar es Salaam kutoka Dodoma, Rais Dkt Magufuli ilifuta uamuzi huo huku akisema ungezuia watanzania wengi kuoana kwani watanzania wenye vyeti hivyo ni chini ya asilimia 20.
“Serikali haiwezi kuruhusu sharti hilo kutumika kwa kuwa litawanyima haki ya kuoa na kuolewa Watanzania wengi ambao hawana vyeti vya kuzaliwa, huku utaratibu wa kupata vyeti hivyo ukiwa bado unakabiliwa na changamoto nyingi kwa wanaohitaji” alisema Rais Dkt Magufuli
“Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania msiwe na wasiwasi wowote, endeleeni na utaratibu wenu wa kuoa na kuolewa kama kawaida na kama kuna kifungu chochote cha sheria kinachomlazimisha mtu awe na cheti cha kuzaliwa ndipo aoe ama aolewe nitamuelekeza Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Harrison Mwakyembe apeleke Bungeni kikarekebishwe” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Lakini si Waziri Mwakyembe pekee ambaye agizo lake limewahi kutenguliwa na Rais Dkt Magufuli. Wamo mawaziri wengine watatu ambao walitoa matamko lakini yakabatilishwa na Rais Dkt Magufuli.
Wa kwanza ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Walemavu Jenista Mhagama ambapo Machi 3, 2016 alitangaza kumteua Dkt. Carina Wangwe kuwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii. Lakini muda mfupi baadae waziri huyo alibatilisha agizo hilo.
Baada ya Waziri Mhagama kubatilisha uteuzi huo, Rais Dkt Magufuli alimteua aliyekuwa mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Prof. Godius Kahyarara kushika nafasi hiyo.
Mwingine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), George Simbachawene ambaye agizo lake la kuondolewa wafanyabiashara wadogo maeneo ya mijini lilipingwa.
Agosti 12, 2016 Waziri Simbachawene alitangaza kuwa wamachinga wote maeneo ya mijini waondoke mara moja na pia wasitishe kufanya biashara zao pembezoni mwa barabara na kwamba wapelekwe katika maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya kufanyia biashara zao.
Rais Dkt Magufuli akihutubia katika mkutano wa hadhara jijini Mwanza alitengua uamuzi huo na kusema kuwa machinga wasiondolewe kwenye maeneo wanayofanyia biashara zao. Aidha, Rais Magufuli alisema wanaweza hata kuamua kufunga barabara moja machinga wakafanya shughuli zao hadi hapo watakapopatiwa maeneo mazuri ya kufanyia biashara na si kupelekwa sehemu ambazo hazina wateja.
Waziri wa tatu aliyekumbana na kauli yake kupingwa na Rais Magufuli ni Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye ambaye alisema kuwa ‘brand’ za wasanii zilindwe katika vita dhidi ya dawa za kulevya inayoendelea nchini.
Waziri Nape aliyasema hayo alipokuwa akitoa maoni yake kuhusu wasanii na watangazaji waliotajwa katika orodha ya watumiaji, wasambazaji wa dawa za kulevya na hivyo kutakiwa kufika Kituo cha Polisi cha Kati kwa ajili ya mahojiano. Ni rahisi sana kuharibu ‘brand’ ya mtu kwa muda mfupi lakini itakuchukua miaka kuweza kuijenga. Hivyo nasisitiza hekima itumike katika vita hii, alisema Waziri Nape.
Akizungumza katika ukumbi wa Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Dkt Magufuli alitupilia mbali hoja hiyo ya kulinda majina ya wasanii aliposema kuwa kwenye vita ya dawa za kulevya asiangaliwe mtu ni nani, ukubwa wa jina lake au cheo chake kwenye jamii, kila anayehusika achukuliwe hatua.
Kuonyesha msisitizo, Rais Dkt Magufuli alisema kuwa hata mke wake kama anatuhumiwa kuhusika na biashara hiyo, akamatwe kwa sababu madhara ya dawa hizo ni makubwa katika jamii yetu.
Watu mbalimbali waliotoa maoni yao kuhusu uamuzi wa Rais Dkt Magufuli wa jana, waliilaumu serikali kwa kukosa mawasiliano na ushirikiano. Aidha walieleza kuwa baadhi ya viongozi wataogopa kutoa maagizo kutokana na hofu kuwa huenda yakapingwa na kiongozi wa nchi.
from Blogger http://ift.tt/2mdLbh7
via IFTTT
from WordPress http://ift.tt/2mZIkY5
No comments:
Post a Comment